Utamaduni hautenganishi
swahili / la cultura non isola
Kisiwa ni sehemu ya ardhi ambayo huchanua kutoka baharini na kulindwa na bahari, inayokitenga na kufarakana na mabara. Ardhi ya kisiwa inaonekana kuwa imara, pana, ivukwayo na shughuli mbalimbali na safari zifungwazo huko, ambazo zikakibadilisha, zikakiharibu, zikakizeeka.
Ardhi ya kisiwa ni kama maji, imefungwa. Inaweza kukaliwa tena na kugeuzwa iwe mpya. Inaweza kuwa dunia ndani ya dunia, yenye kanuni zake. Tufikirie kwa mfano Atlantis, Utopia, kisiwa cha Robinson Crusoe.
Ni visiwa vingapi na jamii bora za kufikirika ngapi vyenye kuibuka na kuzama kila wakati? Mwanafalsafa Jacques Derrida anaandika:
"Kisiwa ni nini? Hakuna dunia, vipo visiwa tu". Kuwaza juu ya kisiwa kwa hivyo kunatushawishi kufikiria tena ulimwengu tunavyozoea nao, kisiwa kinawakilisha ulimwengu kama sura yake ndogo, ni sitiari ya ulimwengu, mpango wake na uasi dhidi yake.
Kwa hivyo, kisiwa ni mahali na vilevile ni kiolezo. Sifa zake sizo za kijiografia au za kimaumbile tu, zinaonyesha pia athari ya ufundi na utamaduni wa binadamu pia. Kwa hilo, kisiwa ni mahali pa uchunguzi, majaribio na maarifa, ni kiolezo cha tamaduni za kisasa. Inahifadhi maana ya kuwako, hata hivyo inahusishwa na michakato ya kujenga/kujengua utambulisho, ya kuachwa/kuwa mbali, ya kupoteza/kujenga mahusiano: kisiwa ni ile hatari ya kujitenga na kufungwa; kisiwa ni fursa ya kuanzisha na kujenga upya, ya kugundua na kuzaliwa upya, ya kuwa wa zamani na wa kisasa; kisiwa ni mahali pengine kuliko popote, kinaficha hazina au ni mahali pa wale waliotoroka, ni mbinu ya kutafuta furaha.
Kionekanapo kwenye upeo wa macho, kisiwa ni kioo cha sisi huwavyo, ni umbo la kiasili lifanyalo tufadhaike na kupapatika. Michel Tournier analinganisha kisiwa na diastoli na sistoli za moyo wa mwanadamu, yaani ile hali ya moyo kutanuka na kupojaa. Ni mduara wa mazingaombwe ambao hufunga na kulinda. Mahali pa usalama, kamili, yai la ulimwengu, au hata bustani ya Edeni. Kisiwa ni kiini kifunikwacho na maji ya mimba, ni ishara ya umama, ya "kurudi tumboni mwa mama": ule ujuzi wa uanamama/umama, mwenye kufafanuliwa kama mbinu ya kuzalisha utamaduni, ndio unaobeba mtazamo maalum juu ya mambo ya binadamu.
Ukarimu, huruma, ulindaji, utunzaji, zawadi, mshikamano na maisha: hizo ni sifa za kimsingi za utamaduni unaoheshima utofauti, ambazo tunakusudia kushiriki kwa njia ya mradi wetu wa kitamaduni.
Walakini, kisiwa pia ni mahali pa mawazo. Ni wazo linaloumbika na kujitokeza kutoka kwa kina kisichopenyeka, chenye giza, kilichojaa maisha: "Visiwa ni kama fikira. Ni kama jangwa, vinavutia. Ni kama hifadhi, vinapokea hadithi na kukinga wanadamu tangu kutungwa kwa shairi la kwanza " (Maylis de Kerangal)
Kisiwa ni picha, ishara, wazo. Hata hivyo, ni mahali halisi na pa kimwili, penye kutawaliwa na mitiririko ya mahusiano ya watu, na miendo ya waliofika na kuondoka: «Tunaondoka, tunakuja. Kisiwa kinajishawishi chenyewe kuvuka bahari ikizungukayo, kugusa ardhi nyingine » (Jean-Luc Nancy). Kisiwa, kwa kweli, hupenyeka, ni mahali wazi.
Uchunguzi wa uchangamano wa jazanda za kisiwa unamaanisha kugundua visasili na mizizi ya kizamani ya miundo yote ya kimantiki; aidha, unamaanisha kuhamisha kwenye jazanda-mahali kila kitu kinachohitajika kuwazua na kukataa: hali ya ufungwa na upweke, kuwamo katika mtego, mafumbo ya kutisha.
Kisiwa ni ufalme wa maradufu: kufungua/kufunga, kukaribisha/kutenga, uhuru/ufungwa, ukaribu/umbali. Maradufu hayo ya utambulisho yatakuwa msingi wa ratiba ya mradi wa “Procida Mji mkuu wa Utamaduni wa Italia kwa mwaka 2021”, kwa vile kisiwa ni fursa ya kuwa na mtazamo bora ili tuhisi utata unaodumu wa maisha, vita vya milele kati ya kujiona kwetu na haja ya kuonyesha upekee wetu.
Mambo yanayotokea kisiwani, yanayoambatana na kuongoza njia ya ombi hili, yanaunda aina ya ramani ya vitendo na matukio: hakuna mahali popote pa kufikirika ambapo hupata uhalisi, panapopatikana na kugundulikana. Kwenye mazingira na maeneo ya visiwa kuna mahali ambapo maisha ya kila siku, vitu vya maumbile na vya kitamaduni ni zana za utafiti wa binadamu unaobadilika daima.
Miradi ina viwango viwili vya uchunguzi. Katika kiwango cha kwanza, cha mlalo, miradi inaelezea ubunifu wa kisiwa kama unavyoonekana, ambao unajidhihirisha katika maisha na utamaduni. Hata hivyo, njia hii ina kina cha wima ambacho ni kwa kweli kama safari, sura ndogo ya uwezekano wa usasa ambapo wazo la maendeleo, la sayansi na la teknolojia humweka binadamu katikati ya kumbukumbu zake, na kwa hivyo, katikati ya uwezo wake wa kujenga wakati ujao, akizidi ufahamu wake wa kuwa mwenyeji na sio mpitaye tu.
Flavia Aiello e Emiliano Minerba